NAHODHA wa timu ya taifa England, Harry Kane, ameuaga ukapela baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake Katie Goodland baada ya kuwa kwenye uhusiano tangu wakiwa wadogo.
Taarifa za wawili hao kuwa kwenye mipango ya kufunga ndoa zilianza kusambaa mapema mwezi huu, laini wawili hao hawakutana kuweka wazi siku na sehemu ya kufanyia sherehe hiyo.
Hata hivyo walianza kwa kuposti picha zao ambazo wamevaa nguo za harusi, lakini walikuwa bado hawajafunga ndoa.
Lakini mapema june 22 mchezaji huyo ambaye anakipiga katika klabu ya Tottenham, aliamua kutumia ukurasa wake wa Instagram kuthibitisha kwa mashabiki zake kuwa tayari amefunga ndoa.
“Hatimaye nimefunga ndoa na rafiki yangu wa karibu, nakupenda sana Katie Goodland,” aliandika Harry Kane.
Mbali na kuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu, lakini Kane alimvisha pete ya uchumba mrembo huyo Julai 2017 walipokuwa mapumzikoni huko Barbados.
Wana ndoa hao tayari wamefanikiwa kuwa na watoto wawili Ivy Jane Kane pamoja na Vivienne Jane Kane ambaye alizaliwa Agosti mwaka jana.
Mastaa ambao walimpongeza kwa kufunga ndoa ni John Terry, pamoja na nyota wa mchezo wa Gofu, Rory McIlroy, nyota wa zamani wa Liverpool na Tottenham, Jamie Redknapp, mshambuliaji wa zamani wa Tottenham, Robbie Keane na wengine wengi.



No comments:
Post a Comment