Wednesday, 3 July 2019

#SPORTS:Alichokisema Messi Baada Ya Kufungwa Na Brazil

Lionel Messi ameahidi kuendelea kuichezea timu yake ya taifa ya Argentina licha kushindwa tena kuiongoza kutwaa ubingwa wa soka wa Amerika Kusini jana Jumanne baada ya kufungwa mabao 2-0 na mahasimu wao wakubwa, Brazil katika mechi ya nusu fainali.
Nyota huyo wa Barcelona mwenye umri wa miaka 32, ambaye alitangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa baada ya Argentina kufungwa katika fainali ya michuano hiyo ya Copa Amerika mwaka 2016, amesema hana mpango wa kutundika daruga baada ya kipigo cha jana.
"Kama naweza kusaidia kwa njia yoyote, nitaendelea kufanya hivyo. Najisikia vizuri sana kwenye kundi hili," alisema Messi ambaye ameshashinda mara tano tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia ya Ballon d'Or (Mpira wa Dhahabu).
"Hiki ni (kukosi) kizuri, kizazi cha wachezaji wenye talanta ambao wanaonyesha kwamba wanaipenda timu ya taifa.
"Matarajio ya baadaye ni makubwa na wana msingi mzuri, wanachohitaji na kupewa muda."
Messi atapata tena fursa ya kuondokana na balaa lake kwenye mashindano hayo mwakani wakati yatakapofanyika Argentina na Colombia, huku fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 zikikaribia.

No comments:

Post a Comment