Thursday, 4 July 2019

#SPORTS:Van Dijk Anahisiwa Kunyankua Ballon d'Or Ya 2019

Beki wa kati, Virgil van Dijk amedaiwa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda Tuzo ya Ballon d'Or na kuwa mchezaji wa kwanza wa safu ya ulinzi kubeba tuzo hiyo maarufu tangu Fabio Cannavaro alipofanya hivyo mwaka 2006.
Beki huyo wa Liverpool anapewa nafasi kubwa baada ya mpinzani aliyekuwa akitishia nafasi yake, Lionel Messi kushindwa kutamba kwenye Copa America na kutupwa nje ya michuano hiyo na Brazil katika hatua ya nusu fainali.
Messi ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo hiyo, ameshindwa kufunga wala kutoa asisti katika michuano hiyo ya Copa America kabla ya timu yake kukumbana na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu wao hao wa Amerika Kusini.
Van Dijk, alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Liverpool msimu uliopita akiisaidia kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka kwenye Ligi Kuu England.
Na sasa anapewa nafasi kubwa ya kubeba Ballon d'Or hasa baada ya kuifikisha Uholanzi pia kwenye fainali ya Uefa Nations League ambapo walichapwa na Ureno. Akibeba basi atakuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool tangu Michael Owen alipobeba mwaka 2001.

No comments:

Post a Comment